0
Menu
Infos

Sirro: Lissu, Lema warudi nitawalinda

Sirro: Lissu, Lema warudi nitawalinda

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema kama ni kweli Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wana hofu kuhusu maisha yao warudi nchini atawalinda

IGP Sirro alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, Polisi walifanya juhudi kumtafuta Lissu awape taarifa kuhusu tuhuma za kutishiwa maisha lakini hakutoa ushirikiano.

Lema, aliyekimbilia nchini Kenya kwa madai ya kutaka hifadhi ys ukimbizi na Lissu anadaiwa kwenda Ubelgiji.

Kamanda Sirro aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, wanasiasa hao wana dhamira mbaya ya kutaka kuharibu sifa ya Tanzania.

"Tulifanya kila aina ya jitihada ikiwemo kuwasiliana na chama chake kumuomba Lissu kuja kutupatia taarifa lakini bado hakufika, alichoona yeye ni kwenda Ubalozini kukaa huko, angeweza kuja hata na Balozi na kutupatia taarifa juu ya mashaka hayo aliyokuwa nayo," alisema IGP Sirro.

Alisema, tangu Lissu aliporudi nchini na kuingia katika mchakato wa uchaguzi, Jeshi la Polisi lilimpa ulinzi hadi akalipongeza lakini baadae akageuka.

Alisema walichofanya Lissu na mwenzake Lema ni kutaka kutengeneza 'mstuko' kwa wananchi na vibaraka wao kuwa wanatishiwa maisha, suala alilodai kuwa halina mantiki yoyote kwa kuwa Tanzania ni sehemu huru kwa kila mmoja.

IGP Sirro alisema, kama wanasiasa hao wamekuwa salama kwa kipindi chote cha maisha yao nchini iweje waibuke na kudai kuwa kuna watu wanawatishia maisha.

"Kama wameenda kupumzika warudi tuendelee kuijenga nchi yetu, kama wanadai wana hofu nipo tayari kuwapa ulinzi, hii ni nchi yetu wote hakuna haja ya kuogopana" alisema.

Chanzo: HabariLeo