0
Menu
Infos

Siri ya Tanzania kuingia uchumi wa kati yatajwa

Siri ya Tanzania kuingia uchumi wa kati yatajwa

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

IDARA ya Taifa ya Takwimu nchini (NBS) imesema takwinu rasmi ndiyo nguzo kuu iliyoivusha Tanzania kufikia uchumi wa kati na maendeleo makubwa ambayo yamefikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma na kusema kuwa takwimu ndiyo zinaeleza kwa usahihi hatua za maendeleo ambazo Tanzania imefikia.

Dk Chuwa alisema wanaotaka kupinga maendeleo yaliyofikiwa wanapaswa kuja na takwimu kuunga mkono hoja zao, badala ya maneno ambayo hayana uhalisia kitakwimu ukilinganisha na kazi kubwa iliyofanywa na serikali.

Kutokana na hilo, alisema Watanzania kwa ngazi zote wanapaswa kuzingatia takwimu katika shughuli zote wanazofanya na mapato na matumizi wakipima hali ya matumizi waliyofanya kama yanaendana na kazi iliyofanyika au kazi iliyofanyika inalingana na mapato waliyoingiza.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBS, Lora Madete ametaka mipango ya maendeleo kwa ngazi zote ifanywe kwa ushahidi wa kitakwimu zilizokusanywa na lengo la utekelezaji wa miradi hiyo kwa mujibu wa takwimu.

Alisema pamoja na Idara ya Taifa ya Takwimu kukusanya na kuchakata takwimu msisitizo unawekwa kuhakikisha wananchi wanajua na kutumia takwimu kwa shughuli zao za kila siku.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema mchango wa takwimu utumike siyo tu kuhesabu idadi ya maiti kwa migogoro ya kivita Afrika bali zitumike katika kujenga amani na uchumi endelevu.

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya Kigoma, Samson Anga alisema kuwa maamuzi ya mipango ya nchi ikifanywa kwa kufuata takwimu rasmi yana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo na kuondoa umasikini.

Andengenye alisema kuwa takwimu za kiserikali ni muhimu katika kutunga sera, namna serikali inavyohudumia jamii na inaweka uwiano wa namna ya kutekelezwa mipango ya maendeleo kwa watu wake.

Chanzo: HabariLeo