0
Menu
Infos

Serikali yapongezwa kwa hamasa matumizi mazuri ya rasilimali

Serikali yapongezwa kwa hamasa matumizi mazuri ya rasilimali

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

Serikali ya awamu ya tano imepongezwa kwa namna ilivyoweza kuhamasisha watu kufanya kazi kwa bidii pamoja na matumizi mazuri ya rasilimali mbalimbali zilizopo katika taasisi za umma.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe (MU) kilichopo mkoani Morogoro, Profesa Lughano Kusiluka ametoa pongezi hizo alipokuwa anazungumzia mafanikio ya chuo hicho katika awamu ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais DK John Magufuli.

Amesema kupitia hamasa hiyo wamefanikiwa kujenga jengo la kisasa lililogharimu shilingi bilioni 3.1 kwa fedha za ndani zilizokusanywa kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo hicho.

“Jengo hili lina kumbi za miadhara zinazoweza kuchukua watu 600,madarasa manne yanayochukua wanafunzi 400 na ofisi za wafanyakazi zenye uwezo wa kuchukua watu 50 ambapo jumla yake lina uwezo wa kuchukua watu 1050 kwa wakati mmoja” amesema Profesa Lughano.

Aidha,Profesa Lughano amebainisha kuwa lengo la ujenzi wa jengo hilo ni kuhakikisha kila mtanzania anayetaka kujiunga na chuo hicho asikose nafasi ya kusoma kwasababu ya uhaba wa miundombinu.

Chanzo: HabariLeo