0
Menu
Infos

Serikali : Madai ya vikwazo EU ni upotoshaji

D7cc0568725217174173174981e86966.jpeg Serikali : Madai ya vikwazo EU ni upotoshaji

Sat, 21 Nov 2020 Source: HabariLeo

SERIKALI imekanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao zikidai kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya limeazimia kuiwekea Tanzania vikwazo vya kiuchumi na kuifutia misaada ya fedha kwa kile kinachodaiwa kuwa ni tathimini yao ya uchaguzi mkuu kubaini dosari.

Taarifa hiyo imetolewa kwa wakati tofauti na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki sanjari na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga.

Ofisi hizo mbili za serikali zimefafanua huo baada ya kuwapo taarifa katika mitandao ya jamii zikiwanukuu baadhi ya watu wakiwamo Watanzania wakionekana kushabikia taarifa hizo zilizotajwa kuwa ni za uongo.

Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili jana, wameshutumu watu wanaotamani Tanzania iwekewe vikwazo na kutajwa kuwa wanapaswa kuonewa huruma na ikiwezekana kupewa ushauri kutokana na mtazamo huo ambao ni hatari kwa nchi.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki liyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi , Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Sheiba Bulu, imefafanua kwamba habari hizo ni za upotoshaji .

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya wizara, Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya (EPCFA) ilikutana katika kikao cha kawaida na kujadili masuala mbalimbali ndani na nje ya Umoja wa Ulaya.

Kikao hicho kilijadili kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu ikiwa ni utaratibu wa kawaida kwa Bunge la Umoja huo kufanya tathmini kwa kila nchi mshirika baada ya kumaliza uchaguzi mkuu.

“Hivyo taarifa kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya limeazimia kuifutia Tanzania misaada yenye thamani ya shilingi za Tanzania trilioni 1.6 inazopata kila mwaka na mikopo yote iliyoomba katika umoja huo pamoja na mashirika yake siyo za kweli na zinalenga kupotosha umma.

Habari hizo za upotoshaji pia zinaeleza kuwa Tanzania itawekewa vikwazo na kuzuiwa kufanya biashara na Umoja wa Ulaya,” ilisema taarifa hiyo .

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba, kamati hiyo ina wabunge 71 na kati yao waliotoa maoni ni wajumbe watano pekee kati ya wajumbe 71 wa kamati hiyo.

“Bunge la Umoja wa Ulaya lenye wabunge 705 ndilo lenye mamlaka ya kupitisha maazimio yote na siyo kamati,” ilielezwa.

Awali Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga ambaye pia ni Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya, kupitia video fupi, alisema kinachosemwa katika mitandao kuwa Tanzania itawekewa vikwazo vya kiuchumi pamoja na kunyimwa misaada ni uongo .

“Habari hizo ni za uongo na za upotoshaji mkubwa kwa sababu kikao hicho cha kamati ya Bunge hakikutoa azimio lolote badala yake kilitoa nafasi kwa wabunge wachache kutoa maoni yao juu ya hali halisi ilivyo nchini Tanzania baada ya uchaguzi mkuu,” alisema.

Miongoni mwa watu waliozungumza na gazeti hili jana juu ya suala hilo ni mchambuzi wa masuala ya uchumi, Gabriel Mwang’onda aliyesema watu wanaotamani Tanzania iwekewe vikwazo wanatakiwa kuonewa huruma na ikiwezekana kupewa ushauri kwani vikwazo katika uchumi wa nchi ni vibaya na inamaanisha kuondolewa katika ushirika na dunia.

“Ni bahati mbaya sana kuona watu wanashangilia kusikia kuwa nchi yao imewekewa vikwazo na kusimamishiwa misaada. Ikiwa hilo litatokea ina maana watakaoumia ni hao hao wanaoshangilia,” alisema Mwang’onda.

Alifafanua kwamba nchi zote duniani zinategemeana na kwamba vikwazo vya kiuchumi katika nchi au kampuni ndani ya nchi ni kikwazo kwa maendeleo.

Alisema wanaoshangilia vikwazo lazima wajue kuwa Tanzania ni nchi muhimu katika Umoja wa Ulaya hivyo ikitokea kukawa na hitilafu kidogo watapiga kelele kwa sababu wanajua kuwa taifa hilo ni kioo na mhimili kwa mataifa mengine hasa katika kanda za Mashariki, Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.

Chanzo: HabariLeo