0
Menu
Infos

Samia apania gesi asilia, Bwawa la Nyerere vikamilike haraka

Samia apania gesi asilia, Bwawa la Nyerere vikamilike haraka

Wed, 7 Apr 2021 Source: HabariLeo

SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeazimia kuhakikisha mradi ya kusindika gesi asilia (LNG) pamoja na Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, inamalizika kama ilivyokusudiwa.

Rais Samia aliyasema hayo jana Ikulu Dar es Salaam baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara na pamoja na watendaji wa baadhi ya taasisi za umma.

Alisema Mradi wa Umeme katika Bwawa la Nyerere ni urithi wa Tanzania hivyo lazima umalizike kama ilivyokusudiwa na akasisitiza lifanyike kila liwezekanalo kupunguza gharama za kuendesha mradi huo.

“Pale ambapo utalaamu wa ndani unaweza basi utumike vizuri. Mmefanya uamuzi mzuri kwenye ule mradi wa kutoa umeme kutoka kwenye bwawa mpaka Chalinze na kwamba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wanafanya wenyewe,” alieleza Rais Samia.

Alisema shirika hilo itakapoona ujuzi wake utafikia mwisho liombe ujuzi nje kwa kuwa mradi huo ni muhimu kwa nchi.

“Wasisite ku- subcontract ili watu waje wafanye tufikie mahali pazuri kwa sababu pale pana usalama wa nchi yetu. Umeme ule ndio usalama wa nchi yetu,” alisisitiza.

Kwa upande wa Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG), alisema suala hilo sasa imefikia wakati uchukuliwe uamuzi sahihi wa kuuendeleza kwa kuwa limekuwa likiimbiwa wimbo kila siku kama ulivyo Wimbo wa Taifa.

“Suala la mradi wa LNG linakaribiana na wimbo wetu wa taifa, tunaimba LNG mpaka leo. Mimi naingia Makamu wa Rais nilishughulika na hili siku mbili tatu kisha nikaliona misuli yangu midogo nikaliacha. Lakini mpaka leo LNG hatujafikia azma hebu tufikie azma,” alisema Rais Samia akimuagiza Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani.

Alisema ni vyema mradi huo ukaangaliwa kama unajengwa au haujengwi na akina nani wamo na akina nani hawataki utekelezwe.

“Wasitucheleweshe, wenyewe wana interest (maslahi) zao na wana miradi kibao huko nje sasa tukienda kwa mwendo wao watatuchelewesha sisi tuamueni kama tulivyoamua kwenye SGR,” alisisitiza.

Alieleza kuwa katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kulikuwa kuna nia ya kuuvuta nyuma mradi huo, lakini serikali ilisema hapana na kumtumia mkandarasi aliyejitokeza na kuanza kutekeleza mradi.

“Sasa alipoanza wanarudi wenyewe wananyang'anyana wamepata loti hii na wanaomba na loti zingine. Kwa hiyo na hili nalo (LNG) tuamue tunampa nani kwa taratibu zipi hatuna utalaamu tutafute watalaamu waje watusaidie,” alielekeza Rais Samia.

Chanzo: HabariLeo