0
Menu
Infos

Samia: Kodi za dhuluma hapana 

Samia: Kodi za dhuluma hapana 

Wed, 7 Apr 2021 Source: HabariLeo

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema suala la kodi ni tatizo kwa kuwa pamoja na mambo mengine, kuna urasimu mkubwa na dhuluma.

Aliyasema hayo jana Ikulu Dar es Salaam wakati akiwaapisha baadhi ya viongozi aliowateua juzi wakiwemo makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa wizara mbalimbali na wakuu wa taasisi za umma.

Alisema wawekezaji na wafanyabiashara wamekuwa wakilipishwa kodi kwa utaratibu usioeleweka kwa kuwa kuna wakati wanalipishwa sahihi na wakati mwingine halipishwi kodi sahihi.

“Hakuna utaratibu unaoeleweka ambao mtu akifika Tanzania anajua utaratibu wa kodi ni huu, utaratibu wa vibali vya kazi ni huu na mambo mengine utaratibu ni huu, kwa hiyo wametutwika chapa ya hatutabiriki, ukimwuliza mtu kuhusu Tanzania wanasema hawatabiriki, ukienda leo wanakwambia hiki, ukishawekeza wanakuja na mambo mengine,” alisema Rais Samia.

“Kwa hiyo nataka mkayashughulikie haya, juzi tu nilitoa kauli ya kodi, wawekezaji na wafanyabiashara wengi wamempigia katibu wangu na wasaidizi wangu wanasema mwambie Mama tunataka kumuona, atuhakikishie tunataka kurudi Tanzania, kwa hiyo watu wanataka kuja Tanzania lakini kwa mambo yetu watu wanakimbia Tanzania,” alisema.

Kutokana na hilo, alizitaka wizara husika kuhakikisha wanavutia tena wawekezaji na wafanyabiashara kuja Tanzania, wazalishe ajira, mzunguko wa fedha uongezeke na uchumi ukue.

Kutokana na hali hiyo, alimtaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata kuacha matumizi ya mabavu na ubabe katika kukusanya kodi kwa kuwa haisaidii.

Alisema ana takwimu za vikosi kazi vya TRA namna walivyokusanya mapato ambazo zinaonesha haziko endelevu. Alisema watafanikiwa kuwakamua watu kodi kwa kuwatisha kuwafungulia kesi za uhujumu uchumi au kwenda jela, lakini hatimaye mtu huyo anafunga biashara na kufanya idadi ya walipakodi kupungua.

“Linalonishangaza mimi ni kwamba hawa watu mnawapigia makadirio ya miaka mitano au kumi nyuma, lakini anakuja kibali cha ushuru cha TRA (Tax clearance) na kila mwaka anapewa, lakini anaambiwa lipa bilioni hizi, kama alikiuka kwa nini ulimpa kibali cha ushuru, matokeo anashindwa na anafunga biashara kwa kuogopa kwenda jela,” alisema.

Aliongeza “Naomba mkalitazame hili, kodi tunazitaka, na mimi nasema tena mwende mkakusanye kodi, lakini kodi za dhuluma hapana kwa sababu hazitatufikisha mbali, najua kwa maamuzi yangu haya, tutayumba miezi mitatu-minne, tutashuka kidogo, lakini watakaporudi, wakaanza kulipa tena, tutapanda kwa wingi.”

Alisema mambo mengine kuhusu TRA atayazungumza atakapoanza kukutana na sekta mbalimbali.

Chanzo: HabariLeo