0
Menu
Infos

NIMR yatakiwa kuongeza tafiti

6e595b7e4a2a0d62e9f5d73f45e3e072 NIMR yatakiwa kuongeza tafiti

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

TAASISI ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Mwanza imetakiwa kubuni miradi zaidi ya tafiti.

Taasisi hiyo pia imetakiwa kutibu na kudhibiti magonjwa ya binadamu ili kutoa mchango zaidi katika jitihada za taifa za kuzalisha nafasi mpya za ajira kwa vijana.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Dk Emmanuel Kipole wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya taasisi hiyo.

Alisema taasisi hiyo inatakiwa kufanya tafiti za kisayansi zenye kuleta matokeo makubwa katika kutibu na kukinga magonjwa na kuboresha afya za Watanzania.

Dk Kipole alisema taasisi hiyo inatakiwa kufanya tafiti zenye kugundua maarifa mapya katika kutibu, kukinga magonjwa mbalimbali na kusaidia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutunga au kuboresha sera za utoaji wa huduma za afya nchini kwa lengo la kuboresha afya za wananchi.

Aliishukuru NIMR pamoja na serikali katika ugunduzi wa dawa ya Nimcraf pamoja na dawa nyingine zilizosaidia katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Mkuu wa NIMR Mwanza, Dk Safari Kinung'hi alisema taasisi hiyo imefanya tafiti za kuboresha tiba za magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu hasa kwa wagonjwa wanaishi na virusi vya ukimwi.

Hata hivyo, alisema taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto za upungufu wa wafanyakazi katika baadhi ya taluma na uhaba wa fedha za utafiti.

Chanzo: HabariLeo