0
Menu
Infos

NIMR yatakiwa kubuni miradi zaidi ya utafiti

NIMR yatakiwa kubuni miradi zaidi ya utafiti

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

TAASISI ya Taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) kituo cha Mwanza kimetakiwa kuhakikisha kinabuni miradi zaidi ya utafiti pamoja na kutibu na kuthibiti magonjwa ya binadamu ili kutoa mchango zaidi katika jitihada za kuzalisha ajira kwa vijana.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Dk Emmanuel Kipole wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya Taasisi hiyo. Dk Kipole amesema Taasisi hiyo inatakiwa kufanya tafiti za kisayansi zenye kuleta matokeo makubwa katika kutibu na kukinga magonjwa na hatimaye kuboresha afya za Watanzania.

Amesema taasisi hiyo inatakiwa kufanya tafiti zenye kugundua maarifa mapya katika kutibu na kukinga magonjwa mbali mbali na kusaidia wizara ya Afya,kutunga au kuboresha sera za utoaji wa huduma za afya nchini kwa lengo la kuboresha afya za wananchi.

Aliishukuru NIMR pamoja na Serikali katika ugunduzi wa dawa ya NIMCRAF pamoja na dawa zinginr zilizosaidia katika mapambano dhidi ya virusi vya homa ya mapafu ya Korona.

Mkuu wa Taasisi ya NIMR Mwanza, Dr Safari Kinung’hi alisema kituo chao kimetoa mchango mkubwa sana katika kanda ya ziwa katika kupambana na Kichocho pamoja na Minyoo,Malaria na Shinikizo la damu pamoja na kuchangia katika kutafuta mikakati mbali mbali ya kuyadhibiti.

Ameongeza taasisi yao imefanya tafiti za kuboresha tiba za magonjwa ya Kisukari na Shinikizo la damu haswa kwa wagonjwa wanaishi na virusi vya Ukimwi.

Chanzo: HabariLeo