0
Menu
Infos

Mradi ujenzi wa tenki la Maji safi kukamilika mwakani

Mradi ujenzi wa tenki la Maji safi kukamilika mwakani

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

MRADI mkubwa wa ujenzi wa tenki la maji katika kata Buswelu lenye ujazo wa lita milioni tatu unatarajiwa kukamilika mwakani mwezi Juni.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo wa maji,Kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mwanza (MWAUWASA) Leonard Msenyele alisema ujenzi huo ukikamilika utasaidia sana katika utatuzi wa kero ya Maji katika wilaya ya Ilemela na maeneo mbali mbali mkoani hapa.

Alisema mradi huo upo chini ya mtalamu mshauri wa Egis na ICE Tanzania huku mkandarasi mkuu ni kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation(CCECC).

Msenyele alisema mpaka mradi huo kukamilika utagharimu shilingi bilioni 5.1 na wahisani wa mradi ni Serikali ya Tanzania,Benki ya uwekezaji ya ulaya(EIB) na Shirika la maendeleo la Ufarasana(AFB).

Alisema kazi zinazoendelea katika mradi huo kwa sasa ni kuandaa umwagaji wa zege ya awali kuandaa kitako cha tenki,kukusanya mchanga na kokoto pamoja na kuchimba mawe. Msenyele alisema maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni Buswelu,Lukobe,Kigala,Nsumba na Kahama.

Alisema kazi zingine zinazoendelea ni kutengeneza barabara ya kuelekea kwenye tenki na umwagaji wa zege kuta za katika tenki. Mkuu wa wilaya ya Ilemela,Dk Mathias Lalika alisema anaishukuru sana Serikali kwa kuleta mradi huo mkubwa wa maji wilayani kwake.

Chanzo: HabariLeo