0
Menu
Infos

Matumizi ya antibayotiki mengi si sahihi-Prof Makubi

Matumizi ya antibayotiki mengi si sahihi-Prof Makubi

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

SERIKALI imesema kumekuwepo na ongezeko kubwa la matumizi ya dawa za antibayotiki na takribani asilimia 50 ya dawa hizo zinatumika isivyo sahihi.

Aidha wakati mwingine zinatumiwa kutibia mifugo au kuchanganywa kwenye vyakula vya mifugo, kinyume cha taratibu za kitabibu.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi alisema hayo wakati akifungua wiki ya uhamasishaji wa kuzuia usugu wa vimelea vya dawa dhidi ya dawa za antibayotiki kwa mwaka 2020. Wiki hiyo huanza Novemba 18 hadi 24 kwa lengo la kutoa elimu.

Profesa Makubi alisema tafiti zilizofanyika Tanzania zimebainisha kuongezeka kwa kiwango cha usugu wa dawa hizo.

“Mfano, utafiti wa kitaifa uliofanyika juu ya usugu wa dawa za kifua kikuu ilionesha usugu wa dawa kwa wagonjwa wapya asilimia 1.1 na kwa wagonjwa wanaorudia dawa baada ya kupona kuwa na usugu wa asilimia 4,”alisema.

Alisema pia katika kutibu ugonjwa wa malaria usugu wa dawa za Chloroquine na SP ulijitokeza ambapo dawa ya ALU inatumika kwa sasa.

Alisema usugu wa vimelea dhidi ya dawa aina za antibayotiki unawaweka wananchi katika mashaka makubwa ya kupoteza nguvu kazi ya taifa kwa kusababisha vifo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyotibika.

Aidha, alisema umaskini unaongezeka kutokana na kuugua kwa muda mrefu na kutumia dawa za ghali zaidi.

“Madhara mengine ya kuongezeka kwa usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibayotiki ni kuongezeka kwa vifo vya mifugo na uzalishaji hafifu wa chakula. Pia tatizo hili linaigharimu nchi mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika katika kuliletea taifa letu maendeleo,” alisema.

Alisema katika kudhibiti madhara yatokanayo na dawa hizo, viongozi katika ngazi za maamuzi wakiwemo waganga wakuu wa mikoa, waganga wakuu wa wilaya, viongozi sekta ya mifugo na wengine wanapaswa kuandaa mipango ya kusimamia matumizi sahihi ya dawa hizo.

Kadhalika alisema wataalamu hao wanatakiwa kusimamia ubora wa dawa zinazozalishwa nchini na zinazoiingizwa kutoka nje ya nchi na zilizopo sokoni ziwe na viwango vinavyokidhi; kuhakikisha kuwa sheria zetu za usimamizi wa dawa zinafuatwa kikamilifu.

Chanzo: HabariLeo