0
Menu
Infos

Dk Mwinyi kutangaza Baraza la Mawaziri leo

Dk Mwinyi kutangaza Baraza la Mawaziri leo

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo anatarajiwa kutangaza Baraza la Mawaziri ambalo litaashiria kukamilika kwa serikali yake tayari kuanza kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi wa visiwa hivyo.

Tayari Dk Mwinyi amekamilisha uteuzi wa Makamu wa Pili wa Rais ambaye ni Hemed Suleiman Abdalla, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Mwinyi Talib Haji ambao wote ni mara yao ya kwanza kuingia katika Baraza la Wawakilishi pamoja na Baraza la Mawaziri.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wanatarajiwa kupatikana miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi 50 kutoka katika majimbo ya uchaguzi ya Unguja na Pemba pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka katika nafasi 10 za uteuzi wa rais.

Kwa upande wa nafasi 10 za uteuzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Kuteuliwa na Rais, tayari Dk Mwinyi amefanya uteuzi wa kuchagua wajumbe watano akiwamo Makamu wa Pili wa Rais.

Wajumbe wengine ni Tabia Ali Mwita ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa na Juma Ali Khatib ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha Ada Tadea aliyekuwa pia mgombea wa urais katika uchaguzi uliopita.

Wengine ni Sada Mkuya ambaye alipata kuwa Mbunge wa Jimbo la Welezo na Waziri wa Fedha wa Muungano katika kipindi cha Rais mstaafu Jakaya Kikwete, na wa tano ni Anna Atanas.

Kwa mujibu wa tathmini na duru za kisiasa, Baraza la Mawaziri linalotarajiwa leo la Dk Mwinyi litakuwa na sura nyingi mpya ikiwemo vijana ambao wengi ni kutokana katika majimbo ya uchaguzi ya Unguja na Pemba.

Kwa mfano, hadi sasa tayari waliokuwa mawaziri katika Baraza la Mawaziri lililopita wapatao 11 hakuna dalili tena za kurudi katika serikali mpya.

Mawaziri wa zamani ambao hawatarajiwi kuwemo leo ni Balozi Amina (Viwanda na Biashara), Dk Sira Ubwa Mamboya (Mawasiliano na Usafirishaji) na Mohamed Aboud (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais) ambao hawakuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania majimbo au kupata nafasi ya uteuzi wa nafasi 10 za rais.

Wengine ni Balozi Ali Karume (Vijana, Michezo na Sanaa), Salama Aboud Talib (Maji, Nishati na Ardhi) pamoja na Maudline Cyrus Castico (Uwezeshaji Wanawake, Watoto na Wazee).

Wapo mawaziri watatu waliopoteza majimbo yao katika kura za maoni za CCM ambao ni Mahmoud Thabit Kombo (Habari, Utalii na Mambo ya Kale), Khamis Juma Mwalimu (Katiba na Sheria) na Mmanga Mjengo Mjawiri (Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi).

Waliokuwa mawaziri katika serikali iliyopita kutoka vyama vya upinzani ambao hawatarajiwi kuwamo Said Soud ambaye alikuwa Waziri asiye na Wizara Maalumu na Hamad Rashid Mohamed aliyekuwa Waziri wa Afya.

Baadhi ya waliokuwa mawaziri wa serikali iliyopita wanaopewa nafasi kubwa ya kurudi ni Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman ambaye amekuwa katika Baraza la Mawaziri kwa miaka 20 sasa.

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Ikulu), Issa Haji Ussi ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Donge, Khalid Salum Mohamed ambaye kwa nyakati tofauti alipata kuwa Waziri wa Fedha na katika mchakato wa kuwania urais wa Zanzibar alifanikiwa kuingia tatu bora.

Kwa upande wa wanawake, mwenye uwezekano wa kurudi ni Riziki Pemba Juma ambaye ni Mwakilishi kupitia nafasi za wanawake na alikuwa Waziri wa Elimu awamu iliopita; wakati Wawakilishi watano walioteuliwa na Rais wanaopewa nafasi kubwa ya kuibuka na uwaziri au naibu uwaziri ni Saada Mkuya, Talib Mwita na Juma Ali Khatib.

Haijafahamika kuhusu hatma ya nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na maridhiano ya kisiasa huchukuliwa na kiongozi wa upinzani aliyepata wastani wa asilimia 10 ya kura zilizopigwa katika Uchaguzi Mkuu. Mgombea wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amepata kura asilimia 19.

Chanzo: HabariLeo