0
Menu
Infos

Dk Mwinyi asitisha Darajani kuhamishwa

Dk Mwinyi asitisha Darajani kuhamishwa

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesitisha uamuzi uliochukuliwa na uongozi wa Manispaa ya Mji wa Unguja wa kuwahamisha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo katika eneo la Darajani pamoja na Komba Wapya na kuwapeleka eneo la Fuoni Jitimai.

Akizungumza na wafanyabiashara hao pamoja na uongozi wa Baraza la Mji na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana, Dk Mwinyi alisema wakati alipokuwa akinadi Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema atahakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao katika mazingira bora yanayoridhisha.

Aliyataja mazingira bora ni pamoja na kupatiwa vitambulisho ambavyo vitawawezesha kufanya shughuli zao bila usumbufu wa kufukuzwafukuzwa.

''Suala la wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora yasiyokuwa na usumbufu huku wakipatiwa vitambulisho nimelitaja katika Ilani ya uchaguzi wakati wa kipindi cha kampeni, sasa sioni sababu ya kuanza kuwasumbua na kama kutafuta eneo ambalo mnasema hamjalipata hadi sasa njooni kwangu nitawatafutieni,” alisema huku akishangiliwa na wafanyabiashara waliokuwa wamejazana kumsikiliza.

Dk Mwinyi alilazimika kufika katika eneo hilo na kutoa maamuzi hayo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Hassan Khatib kutoa taarifa kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo hayo kuondoka katika muda wa siku tatu ili kupisha kazi nyingine za uimarishaji wa mji wa Unguja.

Mkuu huyo wa mkoa alisema wamelazimika kuwahamisha wafanyabiashara katika baadhi ya maeneo ili kutoa nafasi ya utekelezaji wa miradi ya kuboresha mji wa Zanzibar.

Alisema wafanyabiashara hao wametafutiwa eneo la Fuoni katika uwanja wa Ijitimai kwa ajili ya kufanya biashara zao.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamekuwa wakilalamika kuwa eneo hilo sio rafiki kwa kazi zao kutokana na kuwa mbali na makazi ya wananchi.

''Tumewatafutia eneo la kufanya biashara zao katika uwanja wa Ijitimai Fuoni lakini wanalalamika kwamba mazingira sio rafiki kwa upande wa wateja,'' alisema.

Juzi wafanyabiashara katika eneo la Darajani pamoja na Komba Wapya walifika katika baadhi ya taasisi ikiwamo vyombo vya habari kuwasilisha malalamiko yao baada ya kutakiwa kuondoka katika maeneo yao ya biashara bila ya maelekezo mengine.

''Tumefurahishwa na uamuzi wa Dk Mwinyi wa kusitisha kutuhamisha katika maeneo yetu ya biashara, ni uamuzi sahihi kwa sababu tangazo la mkuu wa mkoa limetutaka kuondoka katika maeneo hayo katika kipindi kifupi sana,'' alisema Haji Juma mfanyabiashara wa nguo za mitumba.

Chanzo: HabariLeo