0
Menu
Infos

Daktari jela mwaka mmoja kwa kuendesha hospitali bila leseni

Daktari jela mwaka mmoja kwa kuendesha hospitali bila leseni

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kifungo cha nje mwaka mmoja daktari wa Dental Clinic, Awadhi Juma kwa masharti ya kutofanya makosa baada ya kupatikana na hatia ya kuendesha hospitali binafsi bila leseni.

Adhabu hiyo ilitolewa jana mahakamani hapo baada ya mshtakiwa huyo kukiri kosa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Luboroga.

Mbali na adhabu hiyo, Juma alilipa Sh milioni tatu baada ya kukiri makosa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) na kumaliza kesi hiyo kwa njia ya majadiliano.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu Luboroga alisema adhabu hiyo ilizingatia hoja ya upande wa utetezi na upande wa mashitaka kuwa mshitakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza.

Pia mahakama hiyo imemwachia huru muuguzi wa hospitali hiyo, Kidawa Ramadhani ambaye alikuwa mshitakiwa katika kesi hiyo baada ya DPP kueleza kwamba hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yake.

Awali wakili wa serikali Mwandamizi, Materus Marandu akimsomea mashtaka Juma alidai kuwa kati ya Mei, 2015 hadi Desemba 4, 2019 eneo la Sinza Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, mshitakiwa huyo aliendesha hospitali binafsi iitwayo Dental Clinic bila leseni.

Chanzo: HabariLeo