0
Menu
Infos

DK Mwinyi atoa sababu kutoteua mawaziri wawili

DK Mwinyi atoa sababu kutoteua mawaziri wawili

Fri, 20 Nov 2020 Source: HabariLeo

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hajateua mawaziri katika wizara mbili kwa kuwa chama kikuu cha upinzani chenye asilimia 19 za kura za urais ACT-Wazalendo hakijawasilisha jina la pendekezo la Makamu wa Kwanza wa Rais.

Dk Mwinyi alitoa ufafanuzi baada kuulizwa ni kwa nini hakutaja majina ya mawaziri wa wizara mbili ambazo ni ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii , Jinsia na Watoto.

Alisema chama cha ACT-Wazalendo waliandikiwa barua wapeleke jina la Makamu wa Kwanza wa Rais na mgao wa nafasi za uwaziri kwa mujibu wa uwiano wa viti vya uwakilishi wa kuchaguliwa.

“Nimeacha nafasi mbili za wizara ya biashara na maendeleo ya viwanda pamoja na afya, ustawi wa jamii na jinsia na watoto....tuwape muda kwa mujibu wa Katiba ingawa hadi sasa hawajaenda kuapishwa wala kujisajili,” alisema.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 chama cha ACT-Wazalendo kimepata majimbo 4 kati ya majimbo 50 ya Unguja na Pemba na kuambulia ushindi wa pili katika kura za urais kwa kupata asilimia 19 ya kura halali.

Mapema Mkurugenzi wa Mawasiliano chama cha ACT-Wazalendo, Salim Bimani alikiri kupokea barua ya kuwataka kuwasilisha jina la Makamu wa Kwanza wa Rais na akasema suala hilo litaamuliwa katika vikao vya juu vya Serikali.

“Tumepokea barua katika chama cha ACT-Wazalendo kututaka kuwasilisha jina la makamo wa kwanza wa rais kwa mujibu wa katiba...tunasubiri vikao vya chama ndiyo vitaamuwa kuhusu hatma ya suala hilo ambapo kisheria bado zipo siku 90,” alisema Bimani.

Chanzo: HabariLeo