0
Menu
Infos

Changamoto zinazoshusha ufaulu wa sekondari nchini zafichuliwa

Changamoto zinazoshusha ufaulu wa sekondari nchini zafichuliwa

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

Kutojua matumizi sahihi ya lugha ya kufundishia na ajali za kitabia zitokanazo na Kundi, au Rika, zimetajwa kuwa miongoni mwao changamoto zinazochangia kushusha ari ya kujisomea na kushuka kwa kiwango cha ufaulu miongoni mwao wanafunzi wa sekondari nchini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Shule Huria ya Ukonga Skillful, Diodorus Tabaro, wakati wa mahafali ya kidato cha nne na QT yaliyofanyika shuleni kwake Ukonga Magereza jijini Dar es Salaam, huku akifichua namna shule hiyo ilivyofanikiwa kupambana na mikakati ya kutokomeza changamoto hizo.

Tabaro, ambaye kitaaluma ni Mwalimu, amesema kwa kuzitambua changamoto hizo, imekuwa rahisi kwa shule yake kukabiliana nazo na kuongeza kuwa wamejipanga vyema kumaliza changamoto hizo mwaka ujao wa masomo sambamba na kupandisha ufaulu.

"Tumejielekeza katika kuziba mianya inayostawisha wanafunzi kuathiriwa na Kundi Rika, huku shule ikitoa mafunzo ya ziada ya lugha ya kufundishia yaani Kiingereza (English Course), Mambo ambayo yamekuwa ndio Siri ya ufaulu mzuri hapa Ukonga Skillful Open School, ambako mwaka jana tulifaulisha kwa asilimia 90 ya wahitimu na wakajiunga vyuo vikuu mbalimbali nchini," alisema Tabaro.

Naye Mgeni rasmi wa mahafali hayo, yaliyohusisha wanafunzi 115, Bryceson Makena, aliwataka wazazi na walezi kuacha kusingizia utandawazi wanapokwama katika kuwajenga watoto wao kimaadili na kuwa sababu ya wengi wao kufeli ama kukatiza masomo.

Makena, ambaye ni Mwalimu, Mshereheshaji na Mhamasisaji maarufu nchini, amesema siri pekee ya kutokomeza Kundi Rika miongoni mwao wanafunzi ni wazazi na walezi kujikita katika malezi bora, yanayohusisha mafunzo ya Imani za kidini.

"Mzazi ni figa kuu na muhimu katika mafiga matatu yanayoelezwa na Falsafa Kongwe ya Elimu. Wazazi wasisingizie utandawazi, kwani wapo vijana wanaomudu kulikwepa Kundi Rika, kutokana na msingi imara wa malezi waliopewa nyumbani," alisema Makena.

Alifafanua kuwa, wanapokwama wazazi nyumbani katika kuwajenga watoto, kazi huwa ngumu kwa walimu mashuleni, huku akiipongeza Ukonga Skillful Open School kwa namna ilivyofanikiwa kubadili fikra za wanafunzi waliokosa alama za kutosha mashuleni mwao na kufeli, kuwa wasomi wazuri wanaofaulu kwa alama za juu shuleni hapo.

Aliipongeza shule hiyo kwa uwekezaji waliofanya katika kutoa kozi za lugha ya Kiingereza, ambayo imekuwa tatizo kwa wanafunzi wengi nchini. Pia alisifu ubora wa miundombinu rafiki iliyopo shuleni hapo, huku akiwapongeza walimu kwa aina ya ufundishaji Bora wanaofanya.

Chanzo: HabariLeo