0
Menu
Infos

CBE yaanda kongamano la kitaaluma kujadili tafiti 80

CBE yaanda kongamano la kitaaluma kujadili tafiti 80

Thu, 19 Nov 2020 Source: HabariLeo

JUMLA ya tafiti 80 zinatarajiwa kuwasilishwa leo kwenye Kongamano la Kitaaluma linaloandaliwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emmanuel Mjema alisema kongamano limelenga kuwasilisha na kujadili matokeo ya tafiti za watafiti ndani na nje ya CBE.

Alisema tafiti hizo zinalenga katika maeneo ya teknolojia kwa maendeleo, biashara ndogondogo, utawala, fedha, uchumi, viwanda, miundombinu, sekta isiyo rasmi, mazingira na elimu.

“Hili ni kongamano la tano la kitaaluma ambalo tumefanya tangu serikali kuhamia Dodoma, kongamano la mwaka huu lina kauli mbiu ya ‘ukuaji wa biashara na uchumi kwa maendeleo endelevu,”alisema.

Profesa Mjema alisema watoa mada wakuu wa kongamano hilo linalotarajiwa kuwa na washiriki 300 ni aliyekuwa Makamu Mkuu cha Chuo cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, Profesa Odass Bilame kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na Godfrey Nyaisa ambaye ni Mtendaji Mkuu wa BRELA.

Alisema washiriki wakuu wa kongamano hilo la kitaaluma watakuwa ni wanataaluma na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara, mashirika ya umma, serikali za mitaa na serikali kuu.

Aidha, Profesa Mjema alisema faida ya kongamano hilo la kitaaluma ni kuibua fursa za biashara, viwanda, uchumi na kilimo katika maendeleo endelevu katika taifa, washiriki kuongeza mtandao kwa kukutana na watu wenye tasnia tofauti.

Alisema pia litasaidia kupanua maarifa ya watafiti na kupata suluhisho la matatizo na kupata mbinu mpya na taarifa ambayo haijachapiswa na kupata taarifa za tafiti kubwa.

Chanzo: HabariLeo